Thursday, June 17, 2010

Ukiamini kwamba unaweza, hakuna litakalokushinda maishani mwako!















Maisha siku zote yanaendeshwa kwa kufuata taratibu na kanuni ambazo mwisho wa siku humfanya mwanadamu kuishi kwa amani na furaha na kuweza kutimiza lengo lake la kuwepo hapa ulimwenguni.

Ifahamike kwamba, kila mtu ana wajibu wake ambao anatakiwa kuutimiza kwa kipindi chote ambacho atakuwa hapa duniani lakini kukamilisha wajibu huo kunawezekana kwa mtu jasiri mwenye imani kwamba hakuna linaloshindikana chini ya jua.

Kuamini huko ni miongoni mwa sababu inayoweza kumfanya mtu akatenda mambo makubwa kiasi cha kumfanya aonekane kuwa ni mtu katika watu ndani ya jamii anayoishi.

Na ndio maana kila ninapozungumzia suala la mafanikio huwa nasisitiza sana kila mtu kuwa na imani kwamba anaweza kufanikiwa kama walivyofanikiwa waliotangulia na kama itatokea akashindwa, nayo itakuwa ni hatua ya kuelekea kwenye mafanikio.

Imani ya mtu inaweza kumfanya akatenda mambo makubwa sana na ndio maana wataalam wa mambo ya saikolojia wanaeleza kwamba, unapotaka kufanya kitu chochote kwanza jenga imani kwamba unaweza! Hiyo itakupa nguvu na kukuwezesha kutimiza lengo ulilokusudia.

Wapo watu waliokuwa masikini sana kiasi kwamba katika fikra za haraka haraka huwezi kudhani kwamba maisha yao yanaweza kubadilika na wakaishi maisha ya kifahari.

Lakini kwa kuwa watu hao walikuwa wakiishi kwa imani kwamba ipo siku, sasa hivi ni miongoni mwa watu wanaotembea vifua mbele kwa mafanikio makubwa waliyoyapata. Hii imekuja baada ya watu hao kuukubali umasikini wao na kuuchukulia kama pointi ya kuanzia kuelekea kwenye utajiri.

Hawakuridhika bali siku zote walipambana huku wakiamini kwamba ipo siku watatoka katika dimbwi la umaskini. Wewe pia unatakiwa kuishi katika mazingira hayo huku ukitanguliza imani katika kila jambo unalolifanya.

Amini unaweza kwani hiyo ni moja ya siri wanayoitumia wengi waliofanikiwa. Waliamini kwamba wanaweza, wakajaribu na hata walipodondoka walisimama na kuendelea kupambana mpaka wakatimiza ndoto zao.

Vivyo hivyo kwako, kama wewe ni mfanyabiashara amini kwamba unaweza kuwa mfanyabiashara maarufu na kwa jitihada zako utafika huko. Kama wewe ni mwanafunzi amini unaweza kufika chuo kikuu na kuwa miongoni mwa wasomi wakubwa nchini kama tu utaweka jitihada zako katika masomo.

Nalazimika kusema haya kutokana na ukweli kwamba, kuna watu ambao wana uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo lakini wameendelea kuishi chini ya kiwango kutokana na udhaifu wa imani zao kwamba wao hawawezi.

Wapo wanafunzi ambao kila siku wanafeli mitihani yao na wanaikubali hali hiyo kwasababu wameshaweka akilini mwao kwamba kufaulu kwao ni ndoto ya mchana na wapo waliopangiwa kufaulu kila siku.

Kuna wakulima ambao wameridhika kuendesha shughuli zao za kilimo kwa kutumia zana duni huku wakiamini kwamba haitatokea siku wao wakatumia matrekta na zana nyinginezo za kisasa. Hizi ni imani potofu ambazo zimekuwa zikiwakwamisha wengi kupiga hatua mbele.

Niseme tu kwamba kwa kutumia kanuni ile ile ya hakuna linaloshindikana chini ya jua, kila mmoja aweke akilini mwake kwamba anaweza bila kujali vizingiti vinavyoweza kujitokeza!

Ni wakati wako sasa kuamini kwamba unaweza kuyabadili maisha yako kwa kuwa, kama utaendelea kuamini kuwa huwezi wakati wenzako wanasonga mbele, utaonekana ni mtu wa ajabu usiyestahili hata kuendelea kuwepo katika ulimwengu huu.

Ishi kwa malengo, weka mikakati ya kutimiza malengo yako, ongeza jitihada katika shughuli zako za kila siku na amini kwamba ipo siku Mungu atakunyooshea mkono na wewe kuwa miongoni mwa watu waliofanikiwa.

Sio wakati wa kuridhika kuishi maisha yaliyotawaliwa na dhana ya siwezi! Hivi kama utaishi kwa dhana hiyo wakati wengine wanaweza huoni kwamba utakuwa na kasoro? Ni vema basi makala haya yakakuzindua na kuanza kutimiza wajibu wako huku ukiamini kwamba UNAWEZA! Waingereza wanasema, ’play your part it can be done’!

No comments:

Post a Comment