Ukishapenda ukapendwa, ziba masikio, maneno ya watu yatakuyumbisha!
Awali ya yote nichukue fursa hii kumshukuru Muumba wa mbingu na ardhi kwa mema yote ambayo amekuwa akinitendea katika kila siku ya maisha yangu.
Hakika Mungu ni mwema na kwa hili mimi na wewe tuna kila sababu ya kumtukuza na kumfurahisha kwa kutenda yale ambayo ametuamrisha na kuachana kabisa na yale ambayo ametukataza.
Mpenzi msomaji wangu, mapenzi ni kitu cha ajabu sana, uajabu wake uko katika mazingira tofauti lakini hili ninalotaka kulieleza leo ni pale mtu anapotokea kumzimikia mtu flani ambaye katika mazingira ya kawaida watu wasingetarajia iwe hivyo.
Nasema haya nikimaanisha kwamba, katika hali ya kawaida tulitarajia binti kutoka katika familia bora mwenye mvuto wa kimapenzi kutokuwa tayari kuwa na uhusiano na mwanaume uchwara asiye na mbele wala nyuma.
Lakini kinyume chake tunashuhudia wasichana wazuri sana ambao mambo yao safi wakitokea kuzimika kwa wanaume ambao ni maskini wa kushinda vijiweni, ukiwauliza wasichana hao watakuambia mioyo yao ndiyo imetokea kuwapenda na hawako tayari kuwakosa.
Miongoni mwa wasichana hao wapo ambao familia zao hufikia hatua ya kuingilia kati na kueleza kuwa, hawako tayari binti yao kuwa katika uhusiano wa kimapenzi au kuolewa na mtu ambaye ni fukara lakini kuonesha mapenzi yalivyo ya ajabu, msichana anaweza kukataa na kueleza kuwa, endapo atalazimishwa kuachana na mwanaume aliyempenda kutoka moyoni mwake, bora ajiue!
Achilia mbali hilo, wapo wanaume ‘handsome’, wenye uwezo kifedha ambao katika mazingira ya kawaida tulitarajia kuwaona wakiwa na wapenzi wakali lakini ashakum si matusi, unakuta kijana huyo yuko na jimama au binti ambaye hana shepu, hana sura yaani yupo yupo tu lakini mwanaume anakuambia kwake ndiyo kafika, hasikii la kuambiwa. Jamani hayo ndiyo mapenzi! Mapenzi haya macho, ukishapenda umependa bila kujali huyo uliyempenda yukoje.
Ndio maana katika mazingira hayo unakuta baadhi ya watu wakiwasema wenzao kutokana na aina ya wapenzi walionao. Utawasikia wakisema maneno kama, “Huyo nanii naye, mwanaume gani sasa yule aliyenaye. Utadhani kalazimisha ampende, yaani na uzuri wake wote kuamua kuolewa naye!” Wapo wanaosema maneno hayo huko mtaani.
Wengine hawaishii kuwateta tu wenzao bali hudiriki hata kuwaambia laivu kwamba, wapenzi walionao hawaendani. Jamani hivi hamjui kwamba kibaya kwako kizuri kwa mwenzako? Tambua kwamba, unayemuona si mzuri kwako wapo wanaomfukuzia lakini hawampati. Ndio maana nasema, ukishatokea kumpenda mtu na ukaamini kwamba naye ana mapenzi ya dhati kwako, ziba masikio wala usisikilize yale watakayoyasema walimwengu.
Lazima iwe hivyo kwasababu, ukiwasikiliza kuna uwezekano mkubwa sana wa kukuyumbisha na hata kama moyo wako ulishaamua kumpenda huyo uliyenaye, ukashangaa unaanza kupingana na moyo na kuhisi huenda kweli hukustahili kuwa naye.
Siku zote walimwengu hawakosi la kusema hivyo si wa kuwapa nafasi sana katika kufanya maamuzi yako hasa linapokuja suala la mapenzi. Si wote ambao watavutiwa na mpenzi uliyenaye, wengine watakwambia umedondoka sehemu ambayo siyo na washakunaku wanaweza kwenda mbele zaidi kumponda laazizi wako kuwa, ni kicheche na ashatembea na watu kibao.
Ni suala la wewe kuwa na msimamo na kuamini katika kile ambacho umeamua. Umeamua kumpenda huyo uliyenaye, usiwape nafasi watu waanze kumjadili, waambie aweje aweje, moyo wako ndiyo umetua kwake.
No comments:
Post a Comment