Saturday, July 17, 2010

Mpe mpenzi wako uhuru wa simu yake, amini hawezi kukusaliti!



Nazungumzia ulimbukeni walionao baadhi ya watu wa kutaka kuwachunga na kuwabana wapenzi wao kupitia simu zao za mkononi.

Tatizo la wapenzi pamoja wanandoa kukorofishana mara kwa mara kutokana na kushutumiana juu utumiaji mbaya wa simu zao za mkononi limekuwa ni sugu sasa katika jamii.

Tatizo hili limesababisha ndoa nyingi kuvunjika, wapenzi wengi kuachana na wangine wakiendelea kuwa katika uhusiano lakini katika hali tete. Wanandoa, wapenzi hawaelewani, hawaaminiani kutokana na simu za mkononi.


"Yaani hii simu kwangu ni kero, mpenzi wangu haniamini kila wakati anahisi namsaliti kupitia simu yangu ya mkononi. Kila nikipigiwa simu lazima aniulize ni nani aliyenipigia. Kila ujumbe anataka kuusoma tena kwa nguvu," anaeleza Fatma H, wa Mabibo jijini Dar .


Ninachotaka kusema leo hii ni kwamba, mnapokuwa katika uhusiano kisha mkafikia hatua ya kufikiriana ndivyo sivyo kwasababu tu ya simu zenu za mkononi ni hatari sana. Kwanini mpenzi wako afikie hatua kwa kufikiria kwamba unamsaliti?

Yawezekana nyendo zako ndizo zinamfanya afikirie hivyo licha ya kwamba wanaume wengine wanakuwa na wivu usio na maana. Yaani wao kila wakati wanawashutumu wapenzi wao kuwa na uhusiano wa kimapenzi na watu wengine hata kama hawana uhakika na kile wanachokifikiria.

Mimi sioni sababu ya kumbana sana mpenzi wako kwa njia ya simu licha ya kwamba wakati mwingine unaweza kufanya hivo kama utabaini kuwa amebadili nyendo zake.

Kikubwa ni wanandoa na wapenzi kupeana uhuru wa kumiliki simu zao. Kitendo cha kudhani kwamba mpenzi wako anatumia simu yake katika kuwasiliana na mahawara zake inaonesha kwamba hakuna uaminifu baina yenu.

Haiwezekani simu ya mwenza wako ikiita tu tayari umeshainyakua na ukikutana na sauti ya jinsia tofauti tu unakosa uaminifu kwa mwenzako.

Jamani, huyo mpenzi wako hana kabisa marafiki wa kiume, hana ndugu wa kiume au wafanyakazi wenzake wa kiume. Kimsingi ukiwa mtu wa kumaindi vitu vidogo vidogo kama hivyo mtakuwa mkikorofishana kila siku na mpenzi wako.

Hata hivyo, kaa ukijua kwamba ni vigumu sana kumchunga mwenza wako kupitia simu yake ya mkononi kwani akiamua kukusaliti anaweza kufanya hivyo bila hata kuhusisha simu yake na wewe usijue.


Aidha, uchunguzi wangu umenidhihirishia kwamba, kikubwa ambacho kimekuwa kikichangia katika hili ni wivu, wivu ambao naamini kabisa hauna lengo la kujenga bali kubomoa.

Nasema hivyo kwasababu, ukichunguza sana utakuta wapenzi na wanandoa wengi ambao hawana uhuru na simu zao wamekuwa wakizozana mara kwa mara. Wamekuwa wakipeana shutuma zisizo na ukweli na motokeo yake kuishi katika mazingira yasiyo mazuri.

Kitu ambacho wengi walio katika uhusiano wa kimapenzi wanatakiwa kukijua kukizingatia ni kujiamini na simu zao kama kweli hawazitumii katika kufanya madhambi. Kama kweli wewe ni mwaminifu kwa mpenzi wako, unatakiwa kujiamini kila unapokuwa karibu naye na wala usioneshe kujishtukia.

Wapo ambao kila wanapokuwa na wapenzi wao, wakipata sms tu, watajificha ili wasome haraka haraka kisha wa-'delete'. Wakipigiwa kama hamjui anayempigia basi atakwenda mbali kuipokea na wengine hulazimika kabisa kuzizima simu zao wanapokuwa na wapenzi wao wakijua wakati wowote bomu linaweza kulipuka.

Hivi unapofanya hivyo unataka mpenzi wako akufikirieje? Utamjengea mazingira gani ili akuamini kwamba hauna mtu mwingine?

Kimsingi kutokujiamini kwako kunaweza kukuharibia ndio maana nasema, kama kweli unampenda huyo uliye naye usiweke mazingira ya usiri kwenye simu yako. Wakati mwingine kuwa tayari kumjibu pale atakapokuuliza ni nani aliyekupigia simu au ujumbe huo unatoka kwa nani. Sio kila mara atakuuliza lakini pale atakapokuuliza mjibu.

No comments:

Post a Comment