Saturday, July 17, 2010

Unashindwaje kumuamini mtu ambaye mnapendana kwa dhati?


Assalam alaikum mpenzi msomaji wangu. Ni wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia safu yetu hii maridhawa ya uwanja wa mapenzi ambapo pamoja na mambo mengine tunazungumzia mada mbalimbali zinazogusa maisha yetu ya kimapenzi.

Natumaini kwamba uko shwari tayari kabisa kusoma kile ambacho nimekuandalia kwa wiki hii. Kama ujuavyo, mapenzi ni miongoni mwa vitu vinavyoweza kumfanya binadamu akaishi maisha ya furaha lakini kwa upande mwingine, mapenzi haya haya ndiyo yamekuwa yakiwaliza watu na kuwafanya washindwe kutimiza majukumu yao ipasavyo.

Wakati hao wakiwa hivyo, wapo ambao wamekufa sababu ya mapenzi, wapo ambao hawataki kusikia kitu kupenda sababu ya namna ambavyo mapenzi yamekuwa yakiwatesa. Huo ndio ukweli wenyewe kwamba mapenzi usipoyapatia, ni sumu na inaweza kukukosesha hata hamu ya kuendelea kuishi.

Hata hivyo, mapenzi ya siku hizi hayana uhalisia, usanii umezidi kuwa mwingi. Matapeli wa mapenzi wamezagaa huko mtaani kiasi kwamba, mtu anaweza kukuambia anakupenda kwa dhati kabisa lakini unaweza kukuta hizo ni porojo tu. Hajakupenda chochote bali kilichomo moyoni mwake ni kukutamani tu kingono.

Ndio maana kuna ambao walipoingia katika mapenzi walidhani wanaingia katika uwanja wa furaha lakini sasa wapo walioishia kuvuliwa nguo na kuachwa huku wengine wakiendelea kuwa katika uhusiano lakini kutoa machozi imekuwa ni sehemu yao na maisha aidha kwa kualitiwa au kuanyiwa mambo flani amambyo si ya kufurahisha tofauti na walivyotarajia.

Hili la wapenzi kusalitiana ni tatizo kubwa sana katika maisha ya sasa ya kimapenzi. Kusalitiana kumekuwa kukiongezeka kila kukicha na ndio maana haipiti siku utasikia fulani kafumaniwa na mke wa mtu, jamaa flani kanaswa akiwa na mke wa mtu. Mazingira haya yanamfanya kila anayeingia katika uhusiano kuhisi anajiingiza katika matatizo kwakuwa anajua kusalitiwa na mpenzi wake ni kitu kinachoweza kutokea wakati wowote.

Leo hii hakuna anayeweza kusimama na kujidai kuwa, mpenzi wake katulia na anamuamini kwa asilimia zote. Kila mmoja ukimuuliza atakuambia anahisi anasalitiwa, anahisi penzi lake linamegwa, kama ni mwanamke ukimuuliza kwanini anahisi hivyo, atakuambia wanaume siku hizi hawaaminiki kwakuwa amekuwa akiona wenzake wakisalitiwa kwa macho yake.

"Mimi siwezi kumuamini kabisa mume wangu, Rahel ambaye ni rafiki yangu na mume wake wakiwa pamoja wanaonesha kupendana sana na Rahel anamuamini kweli mumewe lakini huwezi kuamini mumewe ana vimada nje. Sasa mimi nitamuaminije mume wangu? Kama nitachukulia kwamba mume wangu ni msafi kwa asilimia zote nitakuwa najidanganya tu,"anaeleza Josephine mmoja wa wanawake ambao hawa imani na waume zao.

Hiyo ndiyo halisi iliyopo huko mtaani, kuaminiana hakuna tena na hata akijitokeza mtu na kusema anamuamini mpenzi wake sio maneno kutoka moyoni mwake bali atakuwa anajifanyisha tu. Yaani watu wanaishi ili mradi siku zinakwenda huku kila mmoja akimuwinda mwenzake.

Katika hili naomba niseme kwamba, uaminifu ni kitu cha msingi sana kwa wanandoa na hata wapenzi wa kaiwaida. Unaposhidwa kumuamini mwenza wako mara nyingi sana utakuwa ukidhani kwamba anakusaliti kwa kuwa na mtu mwingine hata kama unavyodhani vinaweza vikakosa ukweli ndani yake hali inayoweza kulikwamisha penzi lenu lisinoge.

Penzi haliwezi kunoga kwakuwa, kushindwa kuwa na imani na mtu unayempenda kunaweza kukufanya ukakosa raha kila anapokuwa mbali na wewe. Si kukosa raha tu anapotoka ama anapokuwa mbali na upeo wa macho yako bali pia anaporudi huwezi kuonesha upendo wako kwake na kuweza kujenga chuki dhidi yake.

Suala la uaminifu limekuwa adimu sana kwa baadhi ya wanandoa. Ni wachache sana ambao ni waaminifu kwa wanandoa wenzao. Lakini sasa, wengine wakipewa uongo tu kwamba mwenza wake ana uhusiano na mtu mwingine anakubali mara moja hata kama habari hizo hazina ukweli wowote, matokeo yake unachukua hatua ambazo zinaweza kuteteresha penzi au ndoa yao.

Niseme tu kwamba, amini kwamba mwenza wako ni mwaminifu kwako na jijengee mazingira ambayo na yeye ataamini kwamba wewe ni mwaminifu kwake. Muamini ili naye akuamini. Epuka sana kufanya mambo ambayo yanaweza kumsababishia mpenzi wako akahisi una uhusiano wa kimpenzi na mtu mwingine.

Waweza kufanya hivyo kwa kuwa makini na maneno yako pamoja na matendo yako ambayo kwa namna moja ama nyingine yanaweza kudhihirisha kwamba sio mwaminifu katika ndoa. Kitendo cha kuchelewa kurudi kazini kila siku bila kuwa na sababu za msingi, kulala nje, kuwa na uhusiano wa karibu na watu jinsia tofauti bila kuwepo na sababu za msingi, kupunguza mapenzi, kutokuwa na heshima ni baadhi ya matendo ambao yanaweza kuonesha kwamba sio mwaminifu hivyo ni vyema ukaepukana navyo.

No comments:

Post a Comment